Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amewaelekeza watendaji wa ofisi yake kufanya ufuatiliaji ili kuwashusha vyeo maafisa utumishi katika taasisi za umma walioshindwa kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hasssan la kuwapandisha vyeo watumishi wenye sifa za kupanda madaraja.
Mchengerwa amesema, afisa utumishi yeyote aliyezembea na kusababisha watumishi wa umma kutopandishwa madaraja achukuliwe hatua kwa kushushwa cheo na kuhamishwa kituo cha kazi ili iwe ni fundisho kwa wengine wanaoshindwa kuwajibika ipasavyo.
Amesema Rais anawajali sana watumishi wa umma na ndio maana alitoa agizo la kuwapandisha vyeo katika kipindi ambacho mijadala ya bajeti bungeni ilikuwa ikiendelea jambo ambalo katika hali ya kawaida isingekuwa rahisi kutekelezeka.
“Rais anatambua kuwa nguzo ya Serikali kiutendaji ni watumishi wa umma hivyo haiwezi kufanya vizuri iwapo haitowajali watumishi wake na ndio maana aliagiza wapandishwe madaraja,” Mchengerwa amefafanua.