Bernard Kamilius Membe alizaliwa Novemba 9, 1953, Rondo, Chiponda, katika mkoa wa Lindi, akiwa ni mtoto wa pili kati wa watoto saba (7) waliozaliwa katika familia ya Mzee Kamillius Anthony Ntachile na Mama Cecilia John Membe.
Bernard Membe ni Mmwera, na kama ilivyo desturi ya Wamwera, watoto hutumia jina la ukoo wa Mama. Hivyo watoto wote saba wa familia hii ya Mzee Kamillius wamekuwa wanatumia jina la upande wa mama yao, Cecilia, yaani Membe.
Elimu
1962 – 1968: Elimu ya msingi katika Shule ya Msingi ya Chiponda, Lindi.
1969 – 1972: Elimu ya Sekondari, (O-level) Namupa Seminary, Lindi
1973 – 1974: Kidato cha tano na sita (A-level) Itaga Seminary, Tabora
1975 – 1980: Aliajiriwa serikalini, Ofisi ya Rais
1981 – 1984: Alipata Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano ya Kimataifa (Bachelor Political Science and International Relations)
1985 – 1989: Aliendelea na ajira yake serikalini katika Ofisi ya Rais
1990 – 1992: Alipata Stashada ya Uchumi, Uhusiano wa Kimataifa na Sheria za Kimataifa (Masters- Economics, International Relations and International Law)
1993 – 1994: Alirudi serikalini kuendelea na kazi kama mchambuzi wa mambo ya ulinzi na usalama
Mafunzo
Kati ya mwaka 1975 na 1976 Bernard Membe alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Oljoro, Arusha kwa mujibu wa sheria ambapo vijana wote waliohitimu kidato cha sita walitakiwa kujiunga kwa muda wa mwaka mmoja.
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo aliajiriwa katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Mwaka 1978, alipata mafunzo ya sheria za jinai na usalama wa nchi, nchini Uingereza. Aidha, mwaka 1980, alipata mafunzo ya siasa, katika Chuo cha Chama cha Mapinduzi (CCM), Kivukoni, Dar es Salaam.
Familia
Mwaka 1986, Membe alifunga ndoa Takatifu na Dorcas Richard Masanche, katika Parokia ya Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam. Membe na Dorcas wamejaliwa kupata watoto watatu, Cecilia, Richard na Denis.
Kazi & Siasa
Membe ametumikia nafasi mbalimbali ikiwemo Kamanda wa Vijana wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, na Katibu wa Secretariati ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Mwaka 2000, aliingia bungeni baada ya kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Mtama, kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Licha ya uchanga wake bungeni, akiwa kama mbunge wa kawaida (back bencher), alikuwa mchangiaji mkubwa wa mijadala inayohusu amani, ulinzi na usalama pamoja na utawala bora.
Mwaka 2005 alichaguliwa tena, lakini tofauti na kipindi cha nyuma, Bernard Membe alianza muhula wa pili wa ubunge, Januari 2006, kama ‘front bencher’ baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.
Kufuatia mabadiliko ya baraza la Mawaziri mnamo mwezi Oktoba, 2006, Membe alihamishwa wizara na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini (sasa ni wizara mbili tofauti). Hata hivyo miezi michache baadaye, Januari 2007, Rais Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa baada ya aliyekuwa anashikilia wadhifa huo, Dkt. Asha Rose Migiro aliteuliwa na Katibu Mkuu Baraza la Umoja wa Kimataifa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa baraza hilo.
Bernard Membe amehudumu katika nafasi hiyo hadi 2015, akiwa ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi mfululizo, akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.
Akiwa katika wizara hiyo Tanzania ilipata ugeni wa viongozi wakubwa duniani kama Rais George W. Bush na Baraka Obama wote wa Marekani, Xi Jinping wa China, Joachim Gauck wa Ujerumani, Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Mwana Mfalme wa Malkia wa Uingereza, na Mwana wa Mfalme wa Japan.
Pia chini ya uongozi Membe Tanzania imefanikiwa kupanua wigo wa mahusiano yake Kaimataifa kwa kufunguwa balozi mpya katika nchi za Malaysia, Brazil, Comoro, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait. Aidha, ilifanikiwa kufungua upya Ubalozi wa Tanzania the Hague, Uholanzi uliofungwa mwaka 1994. Kadhalika Balozi mpya za Brazil, Oman, Uturuki, Kuwait, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Namibia zilifunguliwa hapa nchini.
Tangu mwaka 2006 ameshika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Katibu wa Secretariat ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, CCM2006 – 2011: Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Mwenyekiti Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Februari 28, 2020 alifukuzwa uanachama wa CCM na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo kutokuwa mzuri tangu mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha lakini ilionekana sivyo.
Membe alijiunga na ACT-Wazalendo Julai 15, 2020 na akisema kilichonivutia katika chama cha ACT-Wazalendo ni katiba ya chama hicho na itikadi yake ya kutaka kuleta mabadiliko. Aligombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho akaibuka na kura 81,129 sawa na 0.5% ya kura zote.
Alijiuzulu unachama wake Januari Mosi 2021 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kilele cha mvutano kati yake na chama hicho ulioibuka kutokana na yeye kutofautiana na viongozi wenzake baada ya kusitisha kampeni za urais mwaka 2020.
Oktoba 5, 2021 mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Membe alieleza kuunga mkono utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan huku akidokeza kuwa yupo njiani kurejea nyumbani.
Machi 31, 2022 CCM imetangaza kumpokea Membe na kumrejeshea uanachama wake baada ya kaundika barua za kuomba msamaha zaidi ya mara tatu.
Mei 12, 2023 Membe amefariki dunia mkoani Dar es Salaam akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kairuki.