Makinikia sasa kutosafirishwa nje ya Tanzania

0
35

Serikali imesema kuwa imekubaliana na kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Barrick (Barrick Gold Corporation) kwamba makinikia yote yatachakatwa hapa nchini badala ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya shughuli hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maabara ya upimaji madini kwenye udongo na miamba kwenye mgodi wa Bulyanhulu, Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya amesema kampuni hiyo imeleta teknolojia ya kuchakata makinikia nchini na wanafanya kazi kwa uwazi.

“Uzalishaji wa makinikia kama ilivyokuwa zamani hautakuwa ni mtindo kuendelea mbele, badala yake teknolojia mpya itakuwa inatupa dhahabu nyingi kutoka kwenye makinikia, na kiasi kidogo sana kitakachobaki kitakuwa ni makinikia ya copper [shaba] ambayo nayo hayatakuwa sasa na sababu ya kusafirishwa nje ya nchi,” ameeleza Prof. Manya.

Maabara hiyo iliyofunguliwa wilayani Kahama itawezesha kujua kiasi cha dhahabu kilichopo aridhini kabla ya kuchimba.

Awali Serikali ilisitisha usafirishaji wa makinikia nje ya nchi tangu mwaka 2017/18 kutokana na kubaini wizi na udanganyifu wa kiwango cha dhahabu kinachokuwepo kwenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi.

Aidha, Juni mwaka huu katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa bungeni, alisema Serikali imesharuhusu usafirishaji wa makinikia baada ya kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji mapato.

Send this to a friend