Orodha ya nchi 10 maskini zaidi barani Afrika

0
42

Barani Afrika kuna nchi 54 kila moja ikiwa na kiwango chake cha utajiri, na kwa mantiki hiyo ukizipanga utapata nchi tajiri zaidi hadi iliyo masikini zaidi.

Tovuti ya Business Insider Afrika imetoa orodha ya nchi 10 za Afrika ambazo ni masikini zaidi kwa kuzingatia kigezo za Pato la Taifa (GDP) ‘per capita’ na Pato Ghafi la Taifa (GNI) ‘per capita’.

Kigezo cha GDP kinaangazia thamani ya bidhaa na huduma ndani ya mipaka ya nchi husika (bila kujalisha zimezalishwa na nani) kwa kugawanya kwa idadi ya watu waliopo kwenye nchi hiyo. Aidha, GNI ni pato la raia wa nchi husika bila kujalisha lilipozalishwa. Kwa mfano, kupata pato la Watanzania utachukua pato la Watanzania wa ndani ya nchi unajumlisha na pato la Watanzania waliowekeza au wanaofanya kazi nje ya nchi.

GNI ni kipimo kizuri cha pato la nchi kuliko GDP kwani endapo raia wa kigeni amewekeza nchini, pato lao litahesabiwa kwenye GDP ya Tanzania kwa sababu viwanda vyao vipo hapa, hata kama fedha hizo watazisafirisha baadaye kwenda kwenye nchi zao, lakini GNI inahusisha pato la raia wa nchi husika tu.

Turudi kwenye orodha husika kwa kuzingatia vigezo hivyo;

1. Burundi
Hii si nchi maskini Afrika pekee, lakini duniani kote GPD yake ni TZS milioni 1.7 wakati GNI ni TZS 621,026.

2. Somalia
Imekuwa katika mdororo wa kiusalama kwa muda mrefu sana, na hivyo kupelekea changamoto za kiuchumi. Pato la Taifa ni TZS milioni 2.01 na GNI ni TZS 713,030.

3. Jamhuri ya Afrika ya Kati
Taifa hili limezungukwa na nchi zenye migogoro ya kisiasa na kiuchumi na hivyo kujikuta nayo ikitumbukia kwenye shimo hilo. GDP ya nchi ni TZS milioni 2.3 huku GNI ikiwa ni TZS milioni 1.2.

4. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Nchi hii ina rasilimali zote ambazo zingeweza kuifanya kuwa moja ya mataifa tajiri duniani, lakini ni la nne kwa umasikini Afrika. GDP ya nchi ni TZS milioni 2.6 huku GNI ikiwa ni TZS milioni 1.3.

5. Niger
Taifa hilo la Afrika Magharibi limepakana na Nigeria, Benin, Burkina Faso, Mali, Algeria, Chad na Libya. GDP ya Taifa hili ni TZS milioni 2.9 na GNI ni TZS milioni 1.2.

6. Msumbiji
Kundi la kigaid limekuwa moja ya changmoto kubwa nchini humo likitishia amani na shughuli za kiuchumi. Pato la Taifa ni ni TZS milioni 3 huku GNI ikiwa ni TZS milioni 1.1.

7. Liberia
Hii ni nchi ya Afrika ambayo imekuwa jamhuri kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, hata hivyo uongozi mbaya umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo yake. GDP ni TZS milioni 3.3 na GNI ni TZS milioni 1.2.

8. Malawi
Nchi hii ya Kusini mwa Afrika ina GDP ya TZS milioni 3.6 huku GNI ikiwa ni TZS milioni 1.3.

9. Madagascar
Nchi-kisiwa pekee kwenye orodha hii, ikiwa ni moja ya maeneo machache yenye mandhari mazuri zaidi ya kuvutia duniani. Utajiri wake ni GDP TZS milioni 3.7 na GNI ya TZS milioni 1.1.

10. Chad
Taifa hili la kati mwa Afrika lililoghubikwa na mapigano na vikundi vya waasi pamoja na ukame lina GDP ya TZS milioni 3.7 na GNI ya TZS milioni 1.5.

Licha ya nchi hizi kuwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika, zina tabia zinazofanana ikiwa ni pamoja na mapigano, migogoro ya kisiasa, rushwa, na matumizi mabaya ya mali za umma. Haya yote ni matatizo ya kuletwa na binadamu ambayo yanaweza kutatuliwa kuwa na dhamiri ya dhati.