Rais Samia ahutubia mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu wa Uingereza

0
25

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amehutubia moja ya mikutano maalumu uliotishwa na mawaziri wakuu wa Uingereza na Italia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP 26), unaofanyika hapa Glasgow, Scotland.

Katika mkutano huo uliopewa jina la Action and Solidarity –The Critical Decade Event, Rais Samia ameeleza juhudu zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha inakabiliana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua madhubuti kwenye sekta za nishati, misitu, usafirishaji na nyinginezo.

Aidha, Rais Samia pia ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kushikamana na wadau wengine katika kukabiliana na changamoto za tabianchi.

Wakati huo huo, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa kupambana na Mabadiliko ya tabianchi Green Climate Fund (GCF), Yannick Glermarec na kumshukuru kwa ushirikiano baina ya shirika hilo na Serikali ya Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi Green Climate Fund (GCF), Yannick Glermarec kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa utakaojadili athari za mabadiliko ya tabianchi (COP 26) unaofanyika Glasgow, Scotland leo Novemba 1, 2021.

Amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani zimeathiri shughuli za kiuchumi na ujasiriamali kama vile kilimo, utalii na biashara, hivyo fedha zinazopatikana kutoka katika mfuko huo wa zitasaidia Tanzania kuweza kurekebisha athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa malengo yanayowezesha kutolewa kwake.

Aidha, ametoa wito kwa mfuko huo wa GCF kutathmini na kuondoa urasimu wa kiutendaji ili nchi zinazopaswa kupokea fedha kutoka mfuko huo kuweza kuzipata kwa muda ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kesho Novemba 2, 2021, Rais Samia anatarajiwa kuhutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi wanaoshiriki mkutano huo wa COP 26.

Send this to a friend