Wizi wa Tanzanite washamiri Mererani

0
41

Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa ametoa wiki mbili kwa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa vitendo vya wizi wa madini na rushwa vilivyoshamiri katika migodi wa Tanzanite wilayani Mererani mkoani Manyara.

Mchengerwa ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma ambapo amesema kuwa taarifa za wizi wa madini sio siri kwani zimeenea katika eneo hilo na mkoa wa Arusha.

“Ukifika [Arusha] unapata taarifa ni namna gani wizi mkubwa unaendelea na rushwa imekuwa ikitamalaki kwenye eneo hili,” amesema Mchengerwa.

Ametaka TAKUKURU kufanya uchunguzi ili ifahamike nini kinaendelea kwenye mgodi huo unaomilikiwa na serikali.

Mwaka 2018 aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli alizindua ukuta uliojengwa na jeshi kudhibiti wizi wa madini kwenye eneo hilo na wafanyabiashara wengine kukwepa kulipa kodi. Ukuta huo una urefu wa kilomita 24.5 na upana wa mita mita tatu kwenda juu.

Madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee na yana miaka zaidi milioni 600. Madini hayo yaligunduliwa nchini na Jumanne Mhero mwaka 1967.

Send this to a friend