Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kukerwa na kauli ya waziri wake aliyoitoa kuhusu uingizaji wa sukari nchini kutoka Uganda.
Rais amesema hayo wakati akizungumza kwenye jukwaa la wafanyabiashara kati ya Tanzania na Kenya na kueleza kwamba kauli iliyotolewa na waziri wake haikuwa na mantiki.
“Mhe. Rais [Museveni] amesema hapa aliomba sisi [Tanzania] tununue sukari kwao, lakini walisikia statement [maelezo] ya waziri wetu kwamba ‘hatutanunua, hatutakubali.’ Sasa that was nonsense [hiyo haikuwa na mantiki]. Mhe. Rais tutanunua sukari kutoka Uganda,” amesema Rais Samia Suluhu.
Agisti 2021 Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda alisema wizara haitatoa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kwa sababu baada ya watu wamekuwa wakivitumia kujinufaisha wao.
Rais ametumia nafasi hiyo mbele ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kueleza kwamba wamekubaliana kukuza uwekezaji baina ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote.
Ameeleza pia kipindi cha nyuma kulikuwa na mvutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya na kupelekea bidhaa kutokuingia katika nchi hizo mbili, tatizo ambalo limeisha baada ya kukutana na uongozi wa Kenya na kufanya mazungumzo.
Amesema baada ya mazungumzo hayo, biashara baina ya Tanzania na Kenya imekua mara sita zaidi, na hivyo akawaagiza viongozi wa Tanzania na Uganda kukutana na kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo.