Dkt. Salim atunukiwa tuzo na taasisi ya Misri

0
27

Rais Samia Suluhu Hassan amemkabidhi Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim Tuzo ya Heshima ya Utatuzi wa Migogoro, Demokrasia na haki za Binadamu aliyotunukiwa na Taasisi ya Kemet Butros Ghali (KBG) ya nchini Misri.

Rais amebainisha kuwa taasisi hiyo iliamua kumpatia Dkt. Salim Tuzo hiyo ili kuenzi mchango wake katika Uongozi wa Umoja wa Afrika (OAU) kuanzia mwaka 1989 – 2001. Pia kwa kuonesha jitihada kubwa za kusaidia ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kupigania haki, usawa, umoja, kudumisha ulinzi na usalama katika kuleta maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Taasisi ya KBG imekuwa na utaratibu wa kutoa tuzo mbalimbali kila mwaka na kutambua michango ya watu katika tafiti, elimu, amani, demokrasia pamoja na kujishughulisha na masuala ya kuleta amani na ujuzi.

Dkt. Salim alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia mwaka 1984 hadi 1985. Kabla na baada ya hapo alishika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Send this to a friend