Taarifa ya TFF kuhusu CEO wa Simba, Barbara Gonzalez ‘kuzuiwa’ kuingia uwanjani
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeeleza kusikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na baadhi ya viongozi wa Simba eneo la kuingilia Jukwaa la Watu maalumu (VVIP), Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya mchezo wa Simba SC na Yanga SC.
Taarifa ya TFF imekuja muda mfupi baada ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barabara Gonzalez kulalamika kupitia Twitter kwamba amezuiwa yeye na familia yake kuingia uwanjani.
Ufafanuzi wa TFF umeeleza kwamba Gonzalez alifika eneo hilo akiwa ameongozana na watoto watatu ambao hawaruhusiwi kuingia eneo hilo.
Aidha, TFF imesema watoto hao alioongozana nao walikuwa na kadi za watu wengine walioalikwa kinyume na utaratibu unavyotakiwa.
Barbara aliruhusiwa kuingia lakini TFF imesema alianza kutoa lugha isiyofaa kwa Ofisa wa TFF huku akirekodi video na baadaye kutupa kadi na kuondoka.
Imedaiwa pia kuwa viongozi wa Simba walifanya vurugu katika eneo la kuingilia baada ya kutaka kulazimisha mmoja wa viongozi kuingia bila kadi ya mwaliko.
TFF imesema tukio limeripotiwa kwenye mamlaka husika zilizosimamia mchezo.
Mchezo huo wa watani wa jadi umemalizika kwa timu zote kutoka suluhu.