Serikali yatangaza sifa 8 za mtu anayestahili kuwa dalali wa nyumba

0
39

Serikali imetoa mwongozo wa utendaji kazi wa madalali ambao unamtaka kila dalali wa nyumba, majengo, viwanja na mashamba kusajiliwa, usajili unaotarajiwa kuanza Januari 2022.

Waziri wa Nyumba na Maendelelo ya Makazi, William Lukuvi amezitaja sifa na vigezo ambavo madalali watatambulika kupitia kwavyo kuwa ni, awe raia wa Tanzania, mtu mwenye akili timamu na umri usiopungua miaka 18, anuani au namba ya simu au utambulisho kwa mfumo wa kieletroniki (barua pepe).

Sifa nyingine ni mahali pa kufanyia kazi panapofahamika, kuwa na namba ya mlipa kodi, kitambulisho cha NIDA, pamoja na kuwa na cheti cha utambulisho kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Kupitia mwongozo huo utambuzi wa madalali utafanywa na idara mpya ya mipango miji na mazingira katika miji na katika halmashauri za wilaya’’ amesema Lukuvi.

Aidha, kila mtu au kampuni ya udalali itatakiwa kufuata taratibu ikiwemo kujaza fomu ya maombi ya usajili, kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa na kulipa ada ya utambulisho shilingi 20,000 kwa kila mwaka, na baada ya taratibu kukamilika halmashauri husika itampa mwombaji utambulisho wa kufanya shughuli za udalali wa nyumba, majengo, viwanja na mashamba.

Lukuvi ametahadharisha kuwa dalali haruhusiwi kufanya kazi bila kutambuliwa na halmashauri, kukwepa kodi, kufanya udanganyifu, kupokea malipo tofauti na malipo yaliyotajwa na kushawishi au kushinikiza mmiliki kutoza au kulipa bei tofauti na makubaliano.

Send this to a friend