Waziri Ummy apiga marufuku wakurugenzi kuwashusha vyeo wakuu wa shule kisa matokeo mabaya
Serikali imepiga marufuku tabia ya wakurugenzi wa halmashauri kuwashusha vyeo walimu wakuu wa shule pindi shule zao zinapopata matokeo mabaya.
Marufuku hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, wakati akifungua mkutano wa wakuu wa shule za sekondari nchini mkoani Dar es Salaam.
Ummy amesema inashangaza kuona walimu wakuu wakishushwa vyeo holela na wakurugenzi kila shule inapofanya vibaya wakati mwalimu huyo hajawezeshwa.
“Walimu mmekuwa msaada mkubwa sana kwa maendeleo ya elimu lakini hii tabia ya kuwaonea kwa kuwashusha vyeo imeshamiri na siikubali. Sasa kuanzia sasa sitaki kusikia tabia hii, nitawalinda walimu wangu dhidi ya unyanyasaji wa mtu yeyote,” amesema.
Ameongeza kuwa mtoto anapofeli sio tatizo la mwalimu tu, kila mmoja anajukumu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora, mwalimu, mlezi/mzazi, jamii wote wanahusika, sasa kwanini ahukumiwe mkuu wa shule tu, amehoji Ummy.