Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa imebaini uwepo wa ongezeko la wananchi kupata dalili za mafua, na kueleza kwamba hio huwa ni hali ya kawaida kila mwaka ambayo huchangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama ilivyoshuhudiwa miaka iliyopita.
Taarifa ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichalwe imeeleza kwamba wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu viashiria vya mwenendo wa hali hiyo, na amewataka wananchi wenye kikohozi, mafua, maumivu ya mwili na kuchoka watoe taarifa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapatiwe matibabu stahiki.
Wizara imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO19 ikiwa ni pamoja na kuepuka misongamano, kupata chanjo, kuvaa barakoa, kunawa mikono na kutoa taarifa za viashiria vya magonjwa ya mlipuko.
“Huenda maambukizi ya UVIKO19 yakaongezeka zaidi tunapoelekea mwisho wa mwaka,” ameeleza Dkt. Sichalwe akiwataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.