Mahakama Kuu imetupilia mbali maombi ya Serikali ya kibali cha kukata rufaa kupinga uamuzi wake uliokipa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kufungua shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama kupinga tozo ya miamala ya fedha kwenye simu.
Mahakama imetupilia mbali hoja za Serikali na kukubaliana na hoja za LHRC, kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kuridhia maombi yake ya kufungua shauri hilo la kupinga tozo ni uamuzi mdogo ambao kisheria haukatiwi rufaa.
Septemba 8, mwaka huu Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji John Mgetta, ilikubaliana na maombi ya LHRC ya kibali cha kufungua shauri la maombi ya Mapitio ya Kimahakama kupinga kuwepo kwa tozo katika miamala ya simu.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kutupilia mbali hoja zote tatu za pingamizi la Serikali iliyokuwa ikitaka shauri hilo la maombi ya LHRC ya kibali cha kufungua shauri la kupinga tozo; lisisikilizwe, badala yake litupiliwe mbali kwa madai kuwa yana kasoro za kisheria.
Baada ya uamuzi huo, LHRC ilifungua rasmi shauri hilo ambalo limepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu, John Mgetta (kiongozi), Zahra Maruma na Edwin Kakolaki.
Hata hivyo, Serikali ilifungua maombi ikiomba kibali cha kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuipa kibali LHRC kufungua shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama kupinga tozo.
Chazo: Mwananchi