Mwanamke wa miaka 66 auawa na mfanyakazi wa ndani Arusha

0
15

Mwanamke mkazi wa Njiro, jijini Arusha, Janerose Dewasi (66) ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali na anayedaiwa kuwa mfanyakazi wake wa ndani.

Kamanda wa  Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea mauaji hayo na kueleza kuwa polisi  wanamsaka mfanyakazi huyo ambaye alitoweka baada ya mauaji hayo.

Masejo ameeleza kuwa mwili wa mwanamke huyo aliyekuwa akiishi eneo la Block D unaonesha alipigwa na kitu chenye ncha kali kwenye paji la uso.

”Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa anaishi na mfanyakazi huyo, wao pekee na alimuajiri wiki moja iliyopita,” amesema.

“Hatujui lolote, huyo kijana Boniface alikuwa akimsaidia huyu mama kazi zao na leo tumeshangaa kupata taarifa za kifo cha mama huyu,” amesema mmoja wa majirani.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya mwanamke mwingine, Ruth Mmasi kudaiwa kuuawa na mtoto wake wa kiume Patrick Mmasi (19), eneo la Njiro.

Send this to a friend