Serikali ya Tanzania yaamriwa kumlipa fidia mlemavu wa ngozi aliyekatwa mkono

0
12

Kamati ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRDP) imeiamuru serikali ya #Tanzania kumlipa fidia Mariam Staford (36), mwenye ulemavu wa ngozi, aliyekatwa mkono na watu wasiojulikana Oktoba 17, 2008.

Mariam alivamiwa akiwa amelala nyumbani kwao katika Kijiji cha Ntobee Wilaya ya Ngara mkoani Kagera na kukatwa mkono mmoja, na mwingine uliokuwa umejeruhiwa ulikatwa alipofikishwa hospitali.

Watuhumiwa wa tukio hilo walifikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Kagera mwaka huo huo, lakini waliachiwa kwa maelezo kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.

Kutokana na hatua hiyo, Mariam akaamua kutafuta haki katikakamati hiyo ambapo aliwasilisha malalako dhidi ya Serikali ya Tanzania kwa kutopata haki yake ya msingi kama ibara ya 5,6,8,10,14,15(1),16 na 17 ya mkataba wa kimataifa wa haki za wenye ulemavu ambao Tanzania ni mwanachama tangu mwaka 2009.

Baada ya kusikiliza pande zote, kamati imeiamuru Serikali kumlipa fidia Mariam, kumgharamia matibabu yake na kutoa visaidizi (vya mikono) vitakavyomfanya aweze kuishi kwa kujitegemea.

Akizungumzia suala hilo Mariam amesema amefurahishwa na hukumu hiyo na kubainisha kuwa hana ugomvi na Serikali anachokihitaji ni haki yake.

Send this to a friend