Rais Samia: Wanaopanga safu tunawaweka alama mapema

0
42

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa mwanachama wa chama hicho ambaye atajihusisha na vitendo visivyokubalika ikiwemo rushwa na kupanga safu za uongozi atawekwa alama mapema na hatopata nafasi za uongozi.

Akizungumza katika kilele cha matembezi ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar amewataka wanachama wa chama hicho waliohudhuria zoezi hilo wengi wao wakiwa vijana kufanya mambo mema kwani watakuwa wanajifanyia wenyewe.

“Na kila jina lako litakapokuja tutasema, mh, huyu? Huyu si alifanya hili na hili na hili. Tayari jina linarudi chini unafutwa,” amesistiza Rais.

Kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho mwaka huu, Mwenyekiti huyo amewataka vijana kujitokea kushiriki kwani wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, huku pia akiwahimiza kutokubali kugeuzwa kuwa ngazi au mtaji wa kisiasa wa watu wengine.

Aidha, amewataka vijana kutokubali kutumika kuleta mpasuko ndani ya chama hicho akisisitiza kwamba uimara wa chama ndio unaowapa wao ujasiri wa kutembea kifua mbele.

“Msitoe fursa kutumiwa kukipasua chama. Jeuri yenu, majidai yenu, kwenda kwenu kifua mbele ni kwa sababu chama kiko imara,” amewatahadharisha.

Januari 12 mwaka huu Zanzibar itaadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu yaliyoondoa utawala wa Sultan visiwani humo.

 

Send this to a friend