Watu 14 wamefariki dunia wilayani Busega mkoani Simiyu baada ya gari la waandishi wa habari lililokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel kugongana na gari la abiria aina ya Hiace.
Akizungumzia ajali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Busega amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa Hiace hiyo ilikuwa ikijaribu kupita gari la mbele yake ndipo ikagongana na gari la waandishi.
Amesema katika eneo la tukio walifariki watu 11 na wengine watatu walifariki baada ya kufikishwa hospitalini. Ameelza zaidi kwamba majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando na Kituo cha Afya cha Nasa.
Gari la waandishi lilikuwa likielekea Ukerewe kwenye ajili ya kazi za mkuu wa mkoa, na baada ya kugongana liliviringika, kitendo kinachodaiwa kusababisha madhara zaidi.
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa wote waliopoteza ndugu na marafiki na Watanzania kwa ujumla huku akiwaombea marehemu wapumzike kwa amani.
“Nimeshtushwa na vifo vya Watu 14 wakiwemo Wanahabari 6 vilivyotokea leo asubuhi baada ya gari lililokuwa katika msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kugonga na Daladala. Poleni Wafiwa, Wanahabari na jamaa wote. Mungu aziweke mahali pema roho za Marehemu na Majeruhi wapone haraka,” ameandika kupitia ukurasa wake wa Twitter.