Askari wa JWTZ adaiwa kumuua baba yake akimtuhumu kuwa ni mchawi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Askari wa JWTZ, Mussa Ndonde (31), mkazi wa Mlandizi mkoani Pwani kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Edward Ndonde (75) kwa kumchoma kwa kisu akimtuhumu kuwa ni mchawi.
Taarifa ya polisi inaeleza kuwa tukio hilo limetokea Januari 12, 2022 saa 03:00 asubuhi huko Mtaa wa Lumbila, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya ambapo Ndonde anadaiwa kumuua mzazi wake kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumkata kiganja cha mkono.
Polisi wameeleza kuwa chanzo cha tukio ni tuhuma za ushirikina kwamba mtuhumiwa anadai kuwa marehemu ni mchawi na anamloga ili asifanikiwe kwenye mambo yake.
Awali mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu majira ya 03:00 asubuhi pasipo kutoa taarifa yoyote ya kwenda Mbeya na kuingia moja kwa moja sebuleni na kuanza kumshambulia kwa kisu na stuli na kupelekea kifo chake.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi wa kitabibu na mtuhumiwa anaendelea kupatiwa matibabu chini ya ulinzi baada kushambuliwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kutokana na tukio alilofanya.