Siku ya mwisho ya Zuhura Yunus BBC
Mtangazaji mashuhuri wa BBC Zuhura Yunus anaondoka kutoka shirika hilo baada ya kulitumikia kwa takriban miaka 14.
Zuhura atatangaza kipindi chake cha mwisho cha Dira ya Dunia majira ya saa tatu Afrika mashariki .
Hata hivyo amebakiza siku kadhaa za likizo kabla ya kuondoka rasmi.
Mtangazaji huyo aliyejiunga na BBC Swahili mwaka 2008 amesema anataka kuutumia muda wake sasa kuendelea na uandishi na mambo mengine nje ya BBC.
Taarifa ya Zuhura kuondoka BBC inakuja miezi kadhaa baada ya kuandika kitabu chake cha wasifu wa Biubwa Amour Zahor mwanaharakati mwanamke wa kisiasa wakati wa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964.
Zuhura alianza kama mtangazaji wa redio na mzalishaji wa vipindi mwaka 2008. Mwaka 2014 alihamia Swahili TV na akawa mwanamke wa kwanza kutangaza Dira ya Dunia TV.
Chanzo: bbcswahili