Tanzania yaomba mkopo wa ujenzi wa SGR

0
21

Benki ya Biashara na Maendeleo imetoa mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1 (sawa na shilingi Trilioni 2.778) hapa nchini na hivi sasa inakamilisha taratibu za kutoa mikopo mingine yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 500 (sawa na shilingi Trilioni 1 na Bilioni 389) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa wakati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo (Trade and Development Bank – TDB), Admassu Tadese.

Rais Magufuli amemshukuru Bw. Tadese kwa mchango mkubwa unaotolewa na TDB kwa maendeleo ya Tanzania tena bila masharti nafuu na amemuomba Bw. Tadese kuongeza mikopo zaidi itakayosaidia utekelezaji wa miradi muhimu na yenye manufaa ya muda mrefu kama vile ujenzi wa reli, mradi wa kuzalisha megawati 359 za umeme katika mto Ruhuji Mkoani Njombe na miradi ya ujenzi wa miundombinu muhimu.

Kwa upande wake Bw. Tadese amesema TDB imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na ameelezea kufurahishwa na mazungumzo yake na Rais Magufuli ambapo ameahidi kuwa benki hiyo itazingatia ombi la kuongeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Tanzania ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway-SGR) katika kipande cha kuanzia Dodoma kuelekea Kanda ya Ziwa na kanda ya Magharibi ambako itaunganisha na nchi jirani zisizokuwa na bahari.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James.