Maduka binafsi ya kwenye maeneo ya hospitali kuondolewa

0
35

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ifikapo Julai Mosi mwaka huu, maduka yote binafsi yaliyopo ndani ya mita 500 kutoka eneo hospitali ili yataondolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema kumekuwa na tabia inayoshangaza watu kukosa dawa kwenye maduka ya hospitali, lakini kwenye maduka ya nje zipo, jambo ambalo limekuwa likiwaumiza wananchi.

“Maduka ya dawa yote ndani ya Mita 500 ndani ya Hospitali yapo kinyume cha sheria kwasababu Hospitali dawa hakuna lakini kwanini maduka ya nje dawa zipo haikubaliki,” amesema Waziri.

Katika hatua nyingine inayolenga kupunguza msongamano wa watu wanaohitaji huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Waziri amesema kwamba wanaandaa utaratibu kuhakikisha kabla mtu hajafika Muhimbili anakuwa amepita kwenye hospitali za rufaa za kanda.

“Mama Samia ameshanielekeza, na tunakwenda kuboresha huduma kwenye Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa na Hospitali za Halmshauri ili Mtu akija Muhimbili aje na jambo ambalo limeshindikana kule chini.”

Akitolea mfano wa hospitali za Dar es Salaam amesema “tumeona hapa Hospitali za Mwananyamala na Temeke zinaleta Wagonjwa Muhimbili eti kwa sababu hawana damu huo ni uzembe hatuwezi kuukubali.”