Lindi: Wanafunzi wakimbilia madarasa mapya, wayakataa ya zamani
Wananchi wa Halmashauri ya Lindi na Mtama wamesema uamuzi wa Serikali wa kujenga shule shikizi katika maeneo yao umekuwa na manufaa kwa sababu kwa kuwaondolea wanafunzi changamoto.
Wamesema ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo utasaidia kukuza ufaulu wa watoto wao kwa kuwa watahudhuria masomo kwa wakati tofauti na hapo awali walipokuwa wakichelewa kufika kutokana na umbali waliokuwa wakitembea.
Madarasa hayo yamejengwa kupitia mradi wa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 ambapo Serikali kupitia Tamisemi ilielekeza TZS bilioni 60 kujengwa madarasa 3,000 katika maeneo mbalimbali nchini yaliyokuwa na uhitaji na changamoto.
Mkazi wa Mawilo, Olga Kiliani amesema katika eneo lao hakukuwa na shule ya uhakika bali watoto wa ngazi ya awali hadi darasa tatu walilazimika kwenda kusoma shule ya Namangale yenye umbali wa kilomita tatu kutoka katika kijiji hicho.
Ameongeza kuwa kwa ushirikiano wa wanakijiji waliamua kujenga darasa la miti, ambalo halikudumu kwa muda mrefu, hawakukata tamaa walijenga tena darasa moja la tofali la kuchoma ambalo halikuwa na miundombinu bora ya kusomea.
“Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi huu wa vyumba vya madarasa ya kisasa, maana lile la awali wakati wa mvua tunakuwa katika wakati mgumu sana, upepo mkali unaezua bati,” amesema Olga.
Mkazi huyo aliongeza kuwa “Sasa hivi hatuna wasiwasi na hofu kwa watoto kusoma, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuboreshea mazingira elimu hasa vijijini.”
Mwalimu Yunus Nangaponi ambaye ni ofisa elimu taaluma wa halmashauri ya Mtama, alisema wamejenga vyumba vya madarasa 20 katika vituo shikizi nane vilivyogawanywa katika madarasa mawili mawili.
“Vituo hivi vimekuwa mkombozi mkubwa kwa watoto hawa hasa ngazi ya awali waliokuwa wanatembea umbali mrefu kwenda katika shule mama ya Namangale. Mfano hapa katika kituo cha Mawilo hadi shule mama kuna kilomita zisizopungua tano,” alisema Mwalimu Nangaponi.
Mkazi wa Mbanja manispaa ya Lindi, Hamida Bakari alisema uamuzi wa kujenga wa madarasa hayo umewaletea ahueni wananchi ambao walikuwawakitoa michango mbalimbali ikiwemo kujitolea katika ujenzi wa madarasa hapo awali.
“Shule imefunguliwa lakini cha kushangaza wanafunzi hawayapendi madarasa ya awali wanayataka mapya kutokana na ubora wake. Watoto wanasoma katika mazingira mazuri na wanafurahi,” alisema.