Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kwamba Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amenusurika kufyatuliwa baada ya yeye mwenyewe (RC) kuzungumzia mambo yanayokwamisha kukamilika kwa miradi ya maendeleo kwenye mkoa huo.
Rais ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi na huduma zinazotolewa na Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere inayojengwa eneo la Kwangwa mkoani humo.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa amemuomba Rais kuwaondoa wakuu wa idara kwenye mkoa huo kwani wamekaa muda mrefu na hivyo wameunda mtandao wa rushwa unaokwamisha wakurugenzi wanapelekwa kwenye mkoa huo.
“Na mkuu wa mkoa leo kama umeota, nilikuwa nikufyatue hapa, lakini umeanza mwenyewe kuyasema, na hii inanionesha kwamba kweli unafuatilia na unafanya kazi,” amesema Rais.
Akizungumza na wananchi, ametumia muda wake mwingi kuonesha namna viongozi wa mkoa huo wanavyokwamisha maendeleo ya mkoa yenye manufaa kwa wananchi kwa kutosimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi, na kusubiri hadi Rais au waziri afanye ziara.
“Inaelekea uongozi mkoa wa Mara hauko imara…Nataka niwaambie hapa, kuna wakuu wa idara ambao watapisha hizo nafasi. Hatuwezi kuendelea na watu wameng’ang’ana hapo, wameiva kwenye wizi, miradi haiendi, kuna kuvutiana, pesa zipo muda mrefu, tunagombana tujenge kwa mbunge, tujenge kwa diwani.”
Ametaja miradi ambayo imekuwa ikisuasua kwa miaka mingi kuwa ni pamoja na hospitali hiyo, mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Bugwema pamoja na miradi ya barabara ambayo baadhi fedha zimetolewa lakini haijakamilika, huku mingine fedha zimetolewa lakini haijaanzwa.
Amewataka viongozi hao kutanguliza mbele maslahi ya wananchi, na wasipofanya hivyo, ikifika mwaka 2024 atakwenda mkoani humo kuwachongea kwa wananchi wasiwachague tena.
Awali akizungumza na wananchi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema serikali imepokea na italifanyia kazi ombi la Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo la kutaka hospitali hiyo iwe na chuo cha mafunzo kwa wahudumu wa afya, ili kumaliza tatizo hilo mkoani humo.
Rais Samia kesho ataendelea na ziara yake mkoani humo ambapo atazungumza na wakazi wa Bunda, kisha ataelekea Butiama.