Shaffih Dauda afungiwa soka kwa miaka mitano, Gantala afungiwa maisha

0
16

Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF na mwanahabari Shaffih Dauda kutojihusisha na shughuli  za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi  kwa kipindi cha miaka mitano pamoja na faini ya shilingi milioni 6.

Katika kikao kilichofanyika Februari 14 na 15, kamati hiyo ilisikiliza mashauri mawili dhidi ya wanafamilia wa mpira wa miguu Shaffih Dauda na Hawaiju Gantala ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Klabu ya Biashara United.

Shaffih Dauda alilalamikiwa kwa kutoa taarifa za uongo na kuchochea umma kupitia mtandao wake wa Instagram kinyume na kifungu cha 73 (4) (a) pamoja na 75(5) vya kanuni za maadili za TFF, pia kukiuka kifungu cha 3(1) cha kanuni za utii za TFF toleo la 2021.

Hata hivyo Dauda alikiri kuchapisha taarifa hiyo, Lakini alidai akaunti yake inaendeshwa na watu wanne tofauti, na wakati taarifa hiyo inachapishwa alikuwa safarini akitokea Cameroon kurudi Dar es salaam, hivyo hakupata nafasi ya kuihariri.

Kwa upande wa Gantala, TFF ilimlalamikia kwa kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika Mahakama ya kawaida, hivyo kushindwa kutii Ibara ya 59(2) ya katiba ya shirikisho la kimataifa la mpira wa miguu (FIFA), ibara ya 66 ya katiba ya TFF toleo la 2019 na kifungu cha 6(1) (a) cha kanuni za maadili za TFF.

Kamati imemfungia Maisha  Gantala kutojihusisha na maswala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi Maisha. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 6(1), (h),73(3),(c) vya kanuni za maadili za TFF.

Send this to a friend