Mambo ya kuzingatia unapotaka kununua gari
Kumiliki gari ni matamanio karibia ya kila mtu kutokana na adha ya usafiri hasa jijini Dar es Salaam, ambako wingi wa watu unafanya usafiri wa umma kuwa na changamoto nyingi zikiwemo hatari ya kuambukizana magonjwa na wizi.
Pengine hivi sasa una wazo la kununua gari, lakini unachotakiwa kujua ni kuwa kuna mambo mengi ya msingi unayotakiwa kujua kabla hujanunua gari au hata unapotaka kuliuza gari lako ununue toleo jipya au gari jingine ili usipate tabu ya kupata mteja.
Baadhi ya mambo yanayopuuzwa na baadaye humgharimu muuzaji wa gari, ni;
Gharama za matengenezo ya gari unalotaka kununua ikiwa ni pamoja na gharama za mafuta ya gari.
Gharama za mafuta ya gari hupanda mwaka hadi mwaka kutokana na huduma mbalimbali zinazohitajika kufanyika kwenye gari hilo, kwani kadri siku zinavyokwenda ndivyo matengenezo ya gari yanavyokuwa makubwa
Kununu toleo jipya la gari
Haishauriwi sana kununua toleo jipya la gari kwa sababu baadhi ya matoleo hutengenezwa na kuyapa muda wa majaribio, ili kufanya maboresho katika toleo lijalo, inashauriwa kununua gari lililotoka miaka 3 iliyopita.
Tambua wakati wa kununua
Sio kila mwezi ni wa kununua magari, inashauriwa miezi mizuri ya kununua gari ni kuanzia mwezi wa 12 mpaka Machi, hii itakusaidia kuokoa kiasi cha fedha kwani miezi hii makampuni mbalimbali yanayouza magari, hutoa ofa ya kushusha bei ili kuuza bidhaa zao.
Fikikiria kuhusu mauzo ya gari lako pindi utakapotaka kuliuza ili ubadilishe gari jingine. Hapa kikubwa kinachoangaliwa ni jina la gari, kuna magari magumu sana kuingia sokoni na kununulika kutokana na upatikanaji wa vifaa vyake pindi gari hilo linapokuwa limeharibika, pia inashauriwa kuzingatia rangi ya gari lako, watu wengi hupendelea magari rangi nyeusi, fedha na nyeupe.
Usiwe na haraka ya kununua gari, fanya utafiti sehemu tofauti, tumia vyanzo mbalimbali vya intaneti na mitandao ya kijamii, watumie watu wanaojua juu ya magari wakushauri juu ya gari unalotaka kununua, usikurupuke.
Ili ulifurahie gari lako na matumizi ya gari lako ambalo umeligharamikia kulipata, ni lazima ufuate njia sahihi wakati wa ununuzi wake.