Rahabu Lugenge anayeishi katika Kijiji cha Lupembe kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, amesimulia mkasa wake wa kupata mimba akiwa mwanafunzi wa sekondari, na furaha aliyonayo baada ya kupata fursa ya kuendelea na masomo.
Rahabu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shule kuendelea na masomo kwa sababu uamuzi huo utawawezesha wasichana kupata fursa ya masomo kama watoto wengine.
Rahabu aliyekuwa anasoma Sekondari ya Wasichana ya Manyunyu alikatisha masomo mwaka 2020 baada ya kupata ujauzito, ikabidi arudi nyumbani.
Anasema alipata mimba kipindi cha likizo ya UVIKO19, kati Machi hadi Juni alipokutana na kijana wa mtaani aliyemshawishi hadi kuanza naye uhusiano.
“Niligundulika nina ujauzito baada ya kupelekwa kituo cha afya kupimwa kwa sababu kulikuwa na utaratibu kabla ya kurejea shuleni lazima upime. Baada ya kugundua nina mimba, nilikwenda shule hivyo hivyo ingawa hawakugundua kwa sababu hawakutupima tena.
Nilishi na ujauzito kuanzia Juni hadi Oktoba bila walimu kufahamu, ingawa lilikuwa kosa lakini nilijikaza kwa sababu niliogopa kurejea nyumbani, wazazi watanichukuliaje? Sikumwambia mama lakini uongozi wa shule ndio uliompigia simu na kumueleza hali halisi,” amesimulia Rahabu.
Amesema baada ya mama yake, Anna Lupembe kupata taarifa mama alisikitika na kumlaumu kwa kitendo kilichomkuta, hata hivyo alimpa moyo na kumuahidi kumlea hadi ajifungue salama.
“Miongoni mwa maumivu nilioyapitia ni wakati wa kujifungua, lakini mchakato huu ulimalizika salama na namshukuru Mungu. Uchungu uliponishika nilikuwa nyumbani, nikapelekwa hospitali, baada ya kufika madaktari wakanipima na kunieleza kuwa njia yangu bado.
“Wakaniambia nipumzike kwanza hospitali, siku ya pili chupa ilivunjika wakaniamisha wodi na kupeleka chumba cha kujifungulia. Wakanipima na kubainika bado njia, hata hivyo ikashauriwa nifanyiwe operesheni ili kuokoa maisha ya mtoto,” anasema Rahabu.
Rahabu anawashauri wenzake kuepuka vishwawishi vya vijana, akisema alipitia wakati mgumu baada ya kushika ujauzito hadi kujifungua.
Anasema ni maumivu yasiyovumilika kwa mhusika mwenyewe hadi kwa wazazi ambao wanaingia gharama ya kuhangaika huku na kule kuhakikisha wanamlea hadi kujifungua salama. Anasema alipoingizwa chumba cha upasuaji, mama yake alihangaika na kuingia gharama ya kununua vifaa vya matibabu.
Kuhusu agizo la Rais Samia kuruhusu wanafunzi kurejea shuleni, alisema alisikia kwenye vyombo vya habari, ndipo alipoanza mchakato wa kufuatilia ikiwemo kumpigia simu mkuu wake wa shule ili kujua hatima yake.
Mama yake amemshukuru Mungu kwa uamuzi wa Rais Samia wa kuwarejea shuleni wanafunzi waliopata changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito, akisema amepokea kwa furaha mchakato huo. Amesema kwa nyakati tofauti binti yake alikuwa akimsumbua akihitaji kurudi shuleni.
“Namshukuru Rais Samia, angekuwa hapa ningemuinamia kwa furaha na shukrani kwake kwa hatua ya kuwarejesha shuleni wanafunzi waliopata changamoto mbalimbali. Naomba salamu hizi za upendo zimfikie,” anasema huku akitokwa na machozi.