Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema lengo la maadhimisho ya Siku ya Wanawake ni kutoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa maazimio ya kitaifa, kikanda na kimataifa yaliyofikiwa na Serikali.
Rais Samia amesema hayo wakati akihutubia wananchi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.
Aidha, Rais Samia amesema uridhiaji na utekelezaji wa mikataba ya maazimio hayo ni ushahidi kuwa taifa letu linaunga mkono jitihada za kimataifa za kukuza usawa wa kijinsia.
Kwa upande mwingine, Rais Samia pia amesema kuwa janga la UVIKO-19 limesababisha kutikisika kwa uchumi hivyo, amewataka wanawake kutumia fursa za kiuchumi zilizojitokeza kutokana na athari za ugonjwa huo ili waweze kunufaika katika kujiletea maendeleo.
Wakati huo huo, Serikali inajenga vituo vya maendeleo ya jamii katika kila wilaya ili kuweza kutoa fursa kwa wananchi kupata mafunzo mbalimbali, kuongeza ujuzi kwa wanawake waweze kuzalisha bidhaa zenye viwango na kupata masoko.