Wasiojulikana wavunja mlango wa msikiti na kuiba jeneza
Watu wasiojulikana wamevunja mlango wa msikiti na kuiba jeneza linalotumika katika shughuli za mazishi kisha kutokomea nalo pasipojulikana.
Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Rivango, Kata ya Mchauru, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara ambapo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Shaban Mohamed amesema tukio hilo limefanyika usiku wa Machi 5 baada ya waumini kusali ibada ya saa mbili usiku.
Mwenyekiti amesema waumini wa msikitiki huo waligundua kutokea kwa wizi huo mara baada ya kuwasili msikitini hapo alfajiri na kukutana na baadhi ya vitu vilivyokuwa kwenye jeneza kama chaga, shuka inayotumika kufunikia jeneza na mswala vikiwa vimetupwa nje ya msikiti .
Aidha, mwenyekiti anaendelea kusema kuwa waumini wa Kiislamu katika kata hiyo wanataraijia kukutana na kufanya dua ya pamoja kuwataka wahusika wa tukio hilo kijisalimisha na kurudisha jeneza hilo mara moja.
“Tutafanya dua ya pamoja na viongozi wote wa dini kuhusu jambo hilo ili matukio kama haya na mengine yasitokee kwenye kata yetu, tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi tuunganishe nguvu zetu kuwasaka na kuwafikisha kwenye mkono wa sharia,” amesema mwenyekiti.
Kwa upande wake Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Masasi, Hamis Baina amesema kuwa amepokea taarifa ya tukio hilo na uongozi wa Kata ya Mchauru na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo.