Pete ya Ndoa ilianza kuvaliwa nchini Ugiriki na Roma, Italia. Kulingana na utamaduni, pete ya harusi kawaida huvaliwa kwenye kidole cha kushoto au cha kulia, ikiwa mvaaji ni mkono wa kushoto, mara nyingi itaenda kwa mkono wa kulia. Uchaguzi wa kidole cha pete unadaiwa kuhusishwa na imani ya kitamaduni inayojulikana kama vena amoris.
Pete kwa wanandoa ni ishara inayoonesha kwamba mtu mmoja amefungamanishwa na mwenzake. Pete hudhihirisha kuwa umepata kibali cha kuunganishwa kwenye nafsi fulani ambayo inamuunganisha na yule mtu akupaye pete.
Baadhi ya wanandoa wamekuwa wakiacha kuvaa pete zao za ndoa huku wakibeba visingizio mbalimbali, wengine wakidai kuwa zinawabana, kupotea, kuchakaa na kushindwa kununua nyingine na hata wengine husema kuwa ni dalili za kuanza kukosekana kwa uaminifu.
Mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kariakoo, George Fupe, mbobezi katika masomo ya ndoa anasema pete ni ishara ya uaminifu kwa wenza wao, na ishara ya amani ya kutumikia. Kwa maana kuwa unapokuwa umeivaa kuna mtu unamtumikia au unamtunza.
“Kitendo cha kutokuvaa pete kwa makusudi ni kosa, kwa sababu ni utambulisho wa nje kwa wanandoa hao. Maaskofu nao wanavaa pete, ni kuonyesha kuwa wamefungamanishwa na Dayosisi zao,” amesema Fupe.
Moja ya sababu zinazotajwa na Mchungaji Irene Msalilwa kutoka kitengo cha Elimu ya Kikristo KKKT Dayosisi ya Iringa na Mchungaji Kiongozi Idara ya Wanawake Upendo Koko, wanasema kuwa kwa wanandoa wa kiume kutokuvaa pete zao za ndoa ni pamoja na kufanya waendelee kuonekana vijana huko barabarani.
“Hapa Iringa tuko jirani na chuo, mwanaume akija chuoni kusoma hana pete anaanza kuwadanganya mabinti, anasema mimi wala sijaoa, ningekuwa nimeoa si ungeona hata alama yoyote, na akishaingia kwenye mahusiano hayo upendo kwenye familia yake unapungua ama kuisha kabisa,” amesema Upendo.
Mchungaji Daudi Kiula kutoka Dayosisi ya Kati Singida, anabainisha baadhi ya madhara mbalimbali ya kutokuvaa pete kwa wanandoa na kusema kuwa kinachofanyika katika ulimwengu wa mwili kipo pia katika ulimwengu wa roho, hivyo unapoacha kuvaa pete ni kama vile unauambia mwili kuwa hii ndoa si salama.
“Unapoivua ile pete au kuvuliwa na mchepuko, ulimwengu wa roho unakuona kuwa umeingia kwenye uzinzi, na utashangaa pale utakapokuwa unataka kuacha uzinzi unashindwa. Agano ni patano kati ya mtu na mtu, na ndoa ni patano kati ya mtu na mtu pia na Mungu, kwahivyo kuna madhara makubwa ya kutokuvaa pete,” ameeleza Kiula.