Serikali kukamilisha miradi yote iliyopangwa Chato
Rais Samia Suluhu Hassan leo Machi 17 ameongoza mamia ya Watanzania wakiwemo viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini pamoja na wananchi katika maadhimisho ya kumbukizi ya mwaka mmoja ya kifo cha Hayati Dk. John Pombe Magufuli yaliyofanyika Chato Mkoani Geita.
Rais Samia amemuelezea Hayati Magufuli na kusema Serikali itaendeleza mazuri yote yaliyoachwa na Dkt. Magufuli pamoja na kuleta mema mengine mapya.
“Kwa hapa Chato nataka niwahakikishie kwamba miradi yote tuliyopanga na tuliyoanza kuitekeleza itakamilika, nataka niwaahidi wanachato miradi hii itakapokamilika kabisa nitakuja mwenyewe kuifungua kama ambavyo angefanya Rais Magufuli kama angekuwepo,” amesema.
Rais Samia amemwelezea Hayati Magufuli kuwa Kiongozi aliyepinga rushwa na ubadhirifu, na kusisitiza uchapakazi na uzalendo kwa Taifa.
Aidha, Mama Janeth Magufuli amemshukuru kwa dhati Rais Samia kwa kuwa karibu wakati wote toka mumewe afariki pia kuungana pamoja katika maadhimisho hayo licha ya kuwa na majukumu mengi.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amemuelezea Hayati Magufuli kama kiongozi aliyekuwa na busara, mahiri na jasiri na wataendelea kumuenzi kwa kupiga vita vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, mambo ambayo Hayati Magufuli aliyapiga vita.