Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Samwel Mhina (31) mkazi wa Temeke pamoja na wenzake 13 kwa tuhuma za kusambaza video katika mitandao ya kijamii kinyume na sheria.
Mhina ambaye ni mwandishi wa habari na mkurugenzi wa mtandao wa kijamii wa U-Turn Collection na wenzake wanatuhumiwa kusambaza video hiyo ikimuonesha mgonjwa akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Kamanda Muliro Jumanne amesema kwamba “baada ya kusambazwa, Hospitali ya Taifa Muhimbili na wafanyakazi wake walikuwa katika taharuki kubwa.”
Muliro amesema baada ya video hiyo kusambaa na baadhi ya wafanyakazi wa Muhimbili kuhusishwa ililazimisha uchunguzi uanze mara moja ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilifanya uchunguzi huo.
Taarifa ya Muhimbili kuhusu video aliyorekodiwa Prof. Jay
Baada ya watuhumiwa hao kukamatwa na kupekuliwa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kielektroniki zikiwemo kamera, kalama za kiuchunguzi (spying pens), miwani ya kichunguzi, kofia zenye kamera, laptop, memory cards.
“Vyote vinachunguzwa na mamlaka ambazo zipo kisheria ili kutafuta uhusiano kati ya kile kilichotokea cha kusambaza video ile kinyuma na sheria,’ ameeleza kamanda.
Ameongeza kuwa uchunguzi ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.
Licha ya kuwa Muliro hajaweka wazi utambulisho wa mgonjwa aliyerekodiwa, inaaminika kwamba mgonjwa huyo ni mwanamuziki Prof. Jay ambaye hivi karibuni video yake akiwa ICU ilisambaa mitandaoni.
Kusambaa kwa video hiyo kuliibua mjadala mkubwa, huku watu wengi wakionesha kutofurahishwa na kitendo hicho kwani kilikuwa na tafsiri ya kudhalilisha utu wa mtu na kuvunja usiri wa mgonjwa.