Mbowe: CHADEMA haitoshiriki mkutano wa maridhiano wa TCD

0
17

 

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema chama hicho hakitoshiriki makongamano na vikao vyovyote vya Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD) kwa kuwa hawaoni ufumbuzi wa kuipata katiba mpya ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Dar es salaam, Mbowe amesema kuwa kiini cha tatizo katika nchi ni katiba, na tatizo la uvurugaji wa uchaguzi ni Tume ya Uchaguzi, hivyo TCD haina nia ya kuitafuta katiba mpya badala yake ina nia ya kuichelewesha katiba.

“Haya maridhiano yanayozungumzwa kupitia TCD sisi hatukushiriki kuyaandaa, hatuioni nia njema ya kutibu kiu ya watanzania kuhusu katiba. Yametoka matangazo mbalimbali kwamba Mbowe ameridhia, mimi sijaridhia kwenda kwenye vikao vya TCD,” amesema Mbowe.

Aidha, katika hotuba yake amekanusha tetesi zinazoendelea kuhusiana na kuachana na harakati za katiba mpya, baada ya mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu alipoachiwa huru kutoka gerezani.

“Kuna kelele kwamba Mbowe amekwenda Ikulu, Mbowe amekubali katiba isiwepo. Nani kasema maneno hayo?, CHADEMA na Katiba hutotutenganisha, katiba ndio ajenda yetu kuu na tutaipigania kokote,” amesisitiza.

Pia ametumia jukwaa hilo kusema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipeleka majina ya kughushi bungeni na watu wakaapishwa na kutumia fedha za Watanzania.

“Tume ya [Taifa] Uchaguzi leo ni tume ambayo imepeleka majina forgery [ya kughushi] bungeni… Wabunge wameapishwa na kulipwa pesa za Watanzania, forgery [kwa kughushi]. Hawataki kuyazungumza, [wanasema] turidhiane.”

Hata hivyo Mwenyekiti Mbowe amesema kuwa hana kinyongo na yeyote, na CHADEMA iko tayari kufanya mazungumzo na mtu yeyote, chama chochote na mashirika ili kuipata haki wanayoitafuta.

Machi 17 mwaka huu kamati kuu ya CHADEMA ilikutana na kujadiliana mambo kadhaa ikiwemo hatma ya wanachama 19 waliokata rufaa baada ya kufukuzwa uanachama, kupokea ruzuku za serikali na katiba mpya.

Send this to a friend