Spika Tulia: Rais Samia amevuka viwango

0
20

Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson (Mb), amempongeza Rais Samia Suluhu kwa namna alivyoweza kutengeneza rekodi ya kipekee ya uongozi kwa mambo makubwa ya maendeleo aliyoyafanya kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.

Spika ameyasema hayo wakati wa kufungua kongamano la tathmini ya mwaka mmoja ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan lililofanyika leo Machi 19, 2022 katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).

“Hatumpongezi Rais Samia kwakuwa ni mwanamke bali ni kwa ujasiri na uwezo wake binafsi kwamaana kwa tathmini ni kwamba kazi anaiweza na amezidi viwango,” amesema Dkt. Tulia

Aidha amesisitiza kwamba, katika kipindi cha mwaka mmoja Rais Samia ameweza kuimarisha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa miundombinu, uwekezaji pamoja na kukuza demokrasia nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid amesema kuwa imefika muda sasa wananchi wote wakiwemo wale wa vyama vya upinzani kuungana na Serikali katika kujengana na kuacha tabia za kuchochea migogoro isiyo na tija kwa Wananchi kwa kuwa Rais Samia amejipambanua katika haki na usawa wa kila mtu.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini, wasanii na vijana kutoka maeneo tofauti nchini.