Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amemshawishi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwamba pindi miradi ya ujenzi itakapokamilika Rais Samia Suluhu Hassan aandikwe katika moja ya miradi hiyo kama kumbukumbu ya kazi nzuri anayoifanya.
Ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa Daraja la Tanzanite na barabara unganishi uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Dar es salaam na kumwambia Rais kuwa, mambo mengine inabidi asemewe na hawezi kujisemea mwenyewe.
“Sisi Dar es salaam tumeona kuwa, Mheshimiwa Rais kwa kazi hizi nzuri anazozifanya hatumuoni kwenye daraja lolote, hatumuoni kwenye kitu chochote kikubwa akipewa jina. Leo tuko kwenye Tanzanite kuna watu wamepewa madaraja kama akina Kijazi, akina Mfugale kwa kazi kubwa walizozifanya. Miradi iliyobaki hapa Dar ikizinduliwa tuweke jina lako na wewe, kwa kazi nzuri unayoifanya,” amesema.
Aidha, ameendelea kumshawishi Waziri Mbarawa kwa kutaja miundombinnu inayofanywa ikiwemo mradi wa daraja la juu linaojengwa Barabara ya Chang’ombe, au stesheni ya SGR na kusisitiza kuwa kutokana na mazuri aliyofanya Rais Samia wanashauku ya kumlipa kwa kumuweka katika kumbukumbu ya miradi hiyo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza eneo hilo, Rais Samia amewataka Wizara ya Ujenzi kubadilisha alama ya mwenge iliyowekwa kwenye daraja hilo, badala yake watumie alama ya Tanzanite ili kuleta maana halisi ya daraja hilo.