BASATA: Hakuna kujitoa Tuzo za Muziki Tanzania

0
16

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kuwa kwa hatua waliyofikia sasa katika mchakato wa Tuzo za Muziki Tanzania mwaka 2021 ni ngumu kwa msanii yeyote kujitoa.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa, Bona Masenge, amesema kuwa tayari taarifa zao ziko kwenye mfumo na washiriki wote wamekwisha tangazwa, hivyo wananchi wanaendelea na zoezi la upigaji kura.

“Kama kuna changamoto yoyote iliyotokea ni vyema mtu afike BASATA kwa ufafanuzi au kwa uthibitisho kuwa kitu gani kiko kwenye mfumo. Lazima tuwe makini, lazima twende kwa standard za kimataifa, tuwe na msimamo, amesema Bona.

Hata hivyo ameendelea kueleza kuwa mchakato ulitangazwa na watu wote pamoja na wadau wa muziki waliuelewa, pia baraza lilifanya kazi kubwa sana ya kutoa ufafanuzi juu ya tuzo hizo.

“Sisi tuko serious [makini] tunafanya kazi ambayo imekubalika imepata kibali, na lengo ni kutambua mchango wa kazi za sanaa hasa kwenye muziki, serikali iko serious, leo hii zoezi limenoga unajitokeza kuwa unataka kujitoa, ni ngumu sana,” amesisitiza Bona.

Katika taarifa yake amesema kuwa anawapongeza wasanii wote waliochukua nafasi ya kugombea tuzo hizo pamoja na wadau wote, kwani kufikia sasa zaidi ya wapenzi na wadau zaidi ya 40,000 tayari wamepiga kura hivyo zoezi hilo linaendelea vizuri.

Send this to a friend