Ndoa ya Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustino Mrema imeibua utata na kusemekana kuwa ni batili kufuatia uwepo wa madai kuwa mwanamke aliyefunga nae ndoa, Doreen Kimbi, ni mke wa mtu.
Kwa mujibu wa gazeti la Raia Mwema, ndugu wa karibu wa mwanamke huyo amesema hawakupewa taarifa juu ya ndoa hiyo na wameshangazwa kuona picha za ndugu yao akila kiapo cha pili cha ndoa.
Taarifa zinaeleza kuwa Doreen alifunga ndoa na Fredrick Mushi katika Kanisa Katoliki la Kristu Mfalme, Tabata mkoani Dar es Salaam na kujaaliwa mtoto mmoja, na baadaye kushindwa kuendelea na maisha ya ndoa baada ya kudaiwa kuwa mumewe aliondolewa kazini na kushindwa kuihudumia vema familia yake.
“Mwaka 2019 mwanamke baada ya kuona kuwa ndiye anayemlea mume, akamkimbia na kwenda kuishi Moshi ambako alifungua biashara ya maua na upishi, hizo biashara zingine alizosema kwa kweli hatuzifahamu,” alisema ndugu huyo.
Hata hivyo ameendelea kueleza kuwa wanashindwa kuelewa lengo la ndugu yao kuolewa na Mrema, hasa ikizingatiwa kuwa bado hajaachana rasmi na mumewe wa awali kwa mujibu wa taratibu za kanisa.
Kwa mujibu wa ndugu wa Doreen, wanasema wameshangazwa juu ya kauli ya Mrema kuwa alifika nyumbani na kukubaliana kuhusu mahari bila wazazi, kaka na dada zake kujua chochote.
“Hilo la mahari hatujui nani kapokea, kwa sababu huyu ni ndugu yetu lazima tujitokeze kushiriki na kufahamu taratibu gani zimefuatwa kuvunja ndoa yake ya kwanza. Hatujawahi kusikia wala kuhisi kuwa ndugu yetu ataolewa mara ya pili maana alikuwa na uhusiano wa karibu na mumewe wa kwanza,” ameeleza mwanafamilia.
Hata hivyo inaelezwa kuwa katika hafla fupi iliyofanyika baada ya ndoa hiyo iliyofungwa katika Kijiji cha Kiraracha, Marangu, haikuhudhuriwa na ndugu wa damu wa Doreen, isipokuwa marafiki zake wachache.