Bilionea Roman Abramovich apewa ‘sumu’ akisuluhisha Urusi na Ukraine

0
21

Bilionea wa Urusi, Roman Abramovich ameshambuliwa na tatizo la kiafya lililoonesha dalili zinazoashiria huenda alipewa sumu akiwa kwenye mazungumzo ya kumaliza mgogoro kati ya Urusi na Ukraine, katika mpaa wa Ukraine na Belarus mapema mwezi huu, ripoti za karibu zinasema.

Taarifa zinaeleza kuwa mmiliki huyo wa Chelsea FC, ambaye sasa amepona, alipata changamoto za vidonda machoni na ngozi kuchubuka, dalili zilizoonekana pia kwa wapatanishi wawili wa amani wa Ukraine.

Ripoti moja ilisema kuwa madai hayo ya sumu yalipangwa na viongozi wa Urusi wenye msimamo mkali ambao walitaka kuharibu mazungumzo hayo.

Muda mfupi baada ya madai hayo kuibuka, afisa mmoja wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa, alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa taarifa za kijasusi zilidokeza kuwa dalili zao zilitokana na sababu za kimazingira, sio sumu.

Afisa katika ofisi ya Rais wa Ukraine, Ihor Zhovkva, aliambia BBC kwamba ingawa hakuwa amezungumza na Abramovich, wajumbe wa Ukraine walikuwa vizuri na na mmoja alisema hadithi hiyo ilikuwa uongo.

Chanzo kilicho karibu na Abramovich kimeripoti kuwa sasa amepata nafuu na anaendelea na mazungumzo ya kujaribu kumaliza vita nchini Ukraine.

Siku ya Jumapili, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Abramovich amempa msaada ili kukomesha uvamizi wa Urusi nchini humo. Bilionea huyo wa Urusi alisafiri kati ya Moscow na Kyiv kwa vipindi kadhaa vya mazungumzo mwanzoni mwa mwezi.

Abramovich amewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya na Uingereza mapema mwezi huu kutokana na madai ya kuwa na uhusiano na Rais wa Urusi Vladimir Putin, jambo ambalo anakanusha.

Lakini Bw Zelensky ameripotiwa kuiomba Marekani kusitisha kumwekea vikwazo Bw Abramovich, akihoji kuwa anaweza kuchukua jukumu katika mazungumzo ya makubaliano ya amani na Moscow.

Chakula wakati wa mazungumzo

Machi 3 mwaka huu Abramovich aliungana na wasuluhishi wengine katika majadiliano ya amani, na hatua zilizofuata baada ya hapo zimejawa na mkanganyiko mwingi.

Baadaye usiku huo, wajumbe watatu akiwemo Bw Abramovich – kulingana na tovuti ya uchunguzi ya Bellingcat, walipata dalili za sumu ya mishipa ya fahamu. Walikuwa na ngozi iliyovimba, macho kuwashwa na maumivu makali nyuma ya macho, dalili ambazo zilidumu usiku kucha.

Hakuna hata mmoja wao aliyekula chochote kulingana na Bellingcat, zaidi ya chokoleti na maji. Wataalamu wa silaha za kemikali wamechunguza kisa hiki na kuhitimisha kuwa wanaamini kuwa ni matumizi ya kimakusudi ya kemikali. Lakini hawajui ni nani aliyefanya hivyo. Hakuna madai ya kuwajibika.

Bila shaka watu watakuwa wanajiuliza ikiwa hii ilikuwa kazi ya GRU, idara ya ujasusi ya kijeshi ya Urusi, ambayo Uingereza ilihitimisha kuwa ilikuwa nyuma ya sumu ya Novichok Salisbury mnamo 2018.