Serikali kupitia Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki imesema inaangalia namna ya kupunguza utitiri wa tozo kwenye maziwa yanayozalishwa na kusindikwa nchini.
Akizungumza katika mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) jijini Dar es Salaam, Waziri Ndaki ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuondoa tozo kwenye bidhaa zinazotumika kwenye uzalishaji wa maziwa nchini.
Aidha, wizara imeiagiza Bodi ya Maziwa Tanzania (TDP) kushirikiana na TAMPA kuongeza uhitaji wa maziwa kwa wananchi badala ya kutumia nguvu kubwa kusisitiza uzalishaji na usindikaji wa maziwa.
“Nimesikia malalamiko hapa kuwa yale malori yanayotumika kusafirishia maziwa yanatozwa utitiri wa kodi ambazo kwa kiasi kikubwa zinawakwamisha kufanya shughuli zenu, hivyo na hili tutaenda kuliangalia,” amesema Waziri Ndaki
Hata hivyo Mwenyekiti wa TAMPA, Fabian Mwakatuma amesema moja ya tozo inayolalamikiwa na wasindikaji ni ile inayotozwa kwa magari ya kubebea maziwa ambayo yamekuwa yakilazimika kufanya usajili kila mwaka na kulipiwa tozo katika maeneo matatu tofauti ikiwemo TDP, Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA) kwa shilingi 200,000 kila eneo.