Mali za TZS bilioni 5 za mfanyausafi wa Magereza Kenya zashikiliwa
Mahakama Kuu jijini Nairobi, Kenya inashikilia mali zenye thamani ya TZS bilioni 5.2 mali ya mwajiriwa wa Idara ya Magereza nchini humo, anayefanya kazi kama Msimamizi wa Wafanyausafi.
Uamuzi huo umekuja ni baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufungua mashtaka mahakamani ikiomba mali za Eric Kipkurui ikiwemo ardhi yenye thamani ya TZS bilioni 1.14 na magari saba yenye thamani ya TZS milioni 612 vishikiliwe kwa madai kuwa vimepatikana kwa njia zisizo halali.
Mtuhumiwa ametakiwa kuwasilisha nyaraka za umiliki wa mali hizo ndani ya siku saba, na akishindwa kufanya hivyo, mlalamikaji ataruhuiwa kuvitwaa vitu hivyo kwa nguvu kwa lengo la kuvishikilia.
Uchunguzi wa awali umeeleza zaidi kwamba mtuhumiwa ambaye mshahara wake ni TZS 417,980 kwa mwezi alikuwa ana biashara saba ambazo zimesajiliwa kwa jina lake kati ya mwaka 2012 hadi 2016.
Imeelezwa zaidi kwamba katika kipindi hicho cha miaka mitano alitumia biashara hizo kama njia ya kujipatia TZS bilioni 5.2 kutoka Idara ya Magereza kwa kupokea malipo ya bidhaa ambazo hakutoa.
Kesi hiyo imeahirishwa na hadi Oktoba 25, 2022