Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro imemhukumu Bahati Venance (30), mkazi wa Mikocheni TPC kifungo cha maisha jela kwa kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa chekechea mwenye umri wa miaka mitano.
Hukumu hiyo imetolewa Aprili 25 mwaka huu na Hakimu wa mahakama hiyo, Naomi Mwerinde huku Wakili wa Serikali, Nitike Emmanuel akiieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 27, 2021.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali ameeleza kuwa siku ya tukio wakati mtoto alipokuwa akirejea nyumbani alikutana na mshtakiwa ambapo alimpa TZS 500 ili akamnunulie unga dukani, aliporudi ndipo alipomuingiza chumbani na kumfanyia ukatili huo.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi sita akiwemo mmiliki wa chumba kilipofanyika kitendo hicho ambaye alieleza kuwa yeye ndiye mpangaji wa chumba hicho lakini siku ya tukio alikuwa amesafiri na kumwachia mtuhumiwa alale.
Akisoma hukumu yake, Hakimu Mwerinde amesema ushahidi wa upande wa mashtaka ni mzito na haukuacha shaka hivyo mahakama inamhukumu kifungo cha maisha jela ili kutoa fundisho na onyo kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo.