Bodaboda na tuhuma za kubaka na kulawiti wanafunzi Sumbawanga

0
15

Madereva wa pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kikatili vikiwemo kuwabaka, kulawiti na kuwapa mimba wanafunzi hususani wanafunzi wa shule za msingi mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Akizungumza katika mdahalo na waandishi wa habari, Ofisa wa Dawati la Jinsia katika kituo cha polisi mjini Sumbawanga, Winni Dili amebainisha kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi kwamba, watoto wao wamekuwa wakibakwa na wakati mwingine kuingiliwa kinyume na maumbile kwa watoto wa kiume.

“Sio siri watoto wanaumizwa sana tena wakiwa wadogo kabisa wanabakwa na kulawitiwa, hizi taarifa zinaripotiwa katika dawati letu karibu kila siku na tunapofuatiliwa kwa wanaotuhumiwa mara nyingi wanadai sio wao na tunakosa ushahidi wa kuwatia nguvuni, hivyo wanahabari mtusaidie kuelimisha jamii kuhusu suala hili,” amesema.

Ofisa huyo ameongeza kuwa baadhi wa bodaboda hao wamekuwa wakiwakatisha masomo wanafunzi kwa kuwapa mimba na cha kushangaza ni kuwa polisi hawapewi ushirikiano kutoka kwa wazazi ili kuwafikisha mahali husika watuhumiwa hao na badala yake huwaozesha wanafunzi  kinyemela kwa watu hao ambao wengi huwa na umri chini ya miaka 18.

Hata hivyo, Katibu wa bodaboda mkoa wa Rukwa, Willson Mwakibete alikanusha tuhuma hizo na kudai  kuwa  hawajihusishi na vitendo hivyo ila kuna watu ambao siyo bodaboda lakini wanamiliki pikipiki hivyo wananchi wanashindwa kuwatofautisha, wao wamekuwa wakitoa elimu mara kwa mara kwa wenzao wasijihusishe na vitendo vya ukatili.

Send this to a friend