Ripoti ya Polio nchini Malawi yaishtua serikali ya Tanzania

0
32

Ofisa Programu wa Wizara ya Afya katika Mpango wa Taifa wa Chanjo, Lotalia Gadau amesema kampeni ya chanjo ya matone ya polio inatarajiwa kutolewa kuanzia kesho kwa watoto zaidi ya milioni 10 walio chini ya miaka mitano.

Kampeni hiyo inafanyika kwa awamu nne, ya kwanza imefanyika katika mikoa minne iliyopakana na Malawi ambayo ni Njombe, Mbeya, Ruvuma na Songwe na awamu ya pili itaanza siku ya kesho hadi Mei Mosi na itakuwa nyumba kwa nyumba.

“Hii chanjo itatolewa kwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano bila kujali hali zao za chanjo. Kutakuwepo na timu ya uchanjaji na uhamasishaji na itakuwa nyumba kwa nyumba, na chanjo hii haina kitu nyuma yake bali inalenga kumfikia mtoto popote alipo hata kwenye nyumba za ibada,” amesema.

Ofisa huyo amebainisha kuwa mara ya mwisho Tanzania kupata ugonjwa huo ilikuwa mwaka 1996 mkoani Mtwara na mwaka 2015 Tanzania ilipata cheti cha kuonesha hakuna polio nchini kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Kutokana na Malawi kupata hili janga, inatupa wasiwasi kuwa cheti chetu huenda tutanyang’anywa endapo hatutafanya mikakati ya kukabiliana na huu ugonjwa, ndio maana tunaendelea na jitihada kuhakikisha polio haiingii nchini, tumeimarisha chanjo ndiyo maana tangu mwaka 1996 hatujapata kisa,” ameongeza.

Send this to a friend