Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hasara aliyoisababisha ya kukaa nje ya ofisi siku kadhaa katika uzinduzi wa filamu ya Royal Tour nchini Marekani, siyo kubwa ukilinganisha na matokeo ya filamu hiyo itakayoleta mageuzi makubwa nchini na katika Sekta ya Utalii.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha katika uzinduzi wa Royal Tour uliofanyika katika ukumbi wa AICC na kuhudhuriwa na mamia ya watu huku akielezea uzoefu alioupata pindi filamu hiyo inatengenezwa pamoja na uzinduzi alioufanya nchini Marekani.
“Wakati nafanya hili jambo kuna wadogo zangu, wanangu nikawa nasoma kwenye mitandao huko, huyu mama badala ya kufanya kazi amejigeuza Rambo huko. Hasara niliyoisababisha ya kutokukaa ofisini kwa siku nane pamoja na kutokuhudumia wananchi kwa kipindi kile, italipa mara 2000, 3000 kwa kuwa na filamu hii.” amesema Rais Samia
Aidha Rais Samia ameeleza namna alivyokuwa na wasiwasi wakati filamu ikionyeshwa kwa mara ya kwanza na kusema hakuona uzuri wake, alijawa na woga na kufikiri ni kwa jinsi gani watanzania wataipokea, lakini baada ya kutazamwa kila mmoja alisema anataka kuja Tanzania.
Ameeleza kuwa wameanza kuzindua filamu hiyo jijini Arusha kwa kuwa ndipo Utalii ulipojikita na baada ya hapo itafuata Zanzibar tarehe 07 kisha Dar es salaam.