Mwanafunzi mtoro amponza Mtendaji Kata

0
38

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha mahakamani Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nkinga wilayani Igunga, Salama Habibi Ziada kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kwa mzazi ambaye mtoto wake alikuwa mtoro shuleni.
 
Akisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu wa mahakama ya mwanzo Jackline Kessy Wilayani Igunga Mkoa wa Tabora Aprili 28, Mwendesha mashtaka wa Takukuru  Wilaya ya Nzega, Mazengo Joseph ameiambia mahakama kuwa  mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya Rushwa.
 
Ameeleza kuwa Novemba 6, 2021 katika Kijiji cha Ilunga, kata ya Nkinga, mshtakiwa aliomba rushwa ya Sh300,000 kutoka kwa Ndulu Seni Darishi ili asimchukulie hatua mzazi huyo aliyekuwa na mtoto wake anayesoma katika Shule ya Sekondari ya Nkinga kidato cha pili ambaye hakuwa akienda shuleni.
 
Aidha katika shtaka la pili Mazengo ameiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alipokea Rushwa ya shilingi 280,000 kutoka kwa mzazi huyo Novemba 6, 2021.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo hana mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
 
Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 23, 2022 na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Send this to a friend