Baada ya subira ya siku 365 ya wafanyakazi, Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itapandisha mishahara ya watumishi, lakini sio kwa kiwango kilichoombwa naa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma amesema kuwa anafahamu umuhimu wa kuboresha maslahi ya watumishi ili yaweze kuendanana na hali ya maisha ya sasa.
“Ninakubaliana nanyi kabisa kwamba viwango vya sasa [vya mishahara] havikidhi mahitaji ya mfanyakazi na familia yake, hasa kwa wakati wa sasa ambapo gharama za maisha zimepanda,” amesema Rais Samia.
Licha ya ahadi hiyo, Rais Samia hajaweka wazi kuwa ongezeko hilo litakuwa la kiwango gani, lakini amesema mchakato wa hesabu unaendelea na serikali itatangaza karibuni.
“Nimeagiza jambo liwepo [nyongeza ya mishahara], mahesabu yanaendea, tutajua lipo kwa kiasi gani,” ameongeza.
Mbali na ahadi hiyo, Rais ametangaza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua nyingine kuboresha maslahi ya watumishi ikiwemo kupunguza kodi kwenye stahiki zao, kupandisha vyeo/madaraja, kulipa malimbikizo ya watumishi, ajira mpya pamoja na kuboresha mazingira yao ya kazi.