Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Siriel Mchembe amesema kuwa wafanyabiashara wanawagombanisha wananchi na Serikali yao kutokana na kupandisha gharama za bidhaa kiholela na badala yake wananchi wanaitupia lawama Serikali.
Ameeleza kuwa, kutokana na mfumuko wa bei alifanya ziara kwenye masoko na kukubaliana na Maafisa biashara kuwepo na takwimu za bei ya bidhaa kwenye masoko na kama mfanyabiashara atauza bidhaa kwa bei ghali atatakiwa kuonyesha risiti na sehemu aliponunulia.
“Tunachokifanya tutakapokukuta unauza bidhaa kwa bei ghali tutakuuliza umenunua wapi na tunataka risiti na tutakwenda huko alipouziwa, tutalinganisha gharama za kusafirisha bidhaa na bei anayouzia wananchi. Tunapima uwiano huo ili asiumize wananchi na baada ya operesheni hii bei zimeshuka hapa Handeni.” amesema Mkuu wa Wilaya.
Aidha Mkuu huyo ameongeza kuwa wafanyabiashara waliingiwa na tamaa na kuamua kupandisha bei kiholela wakijua kuwa mwananchi lazima atatnunua bidhaa.