Serikali yamnyang’anya mkandarasi wa MV Hapa Kazi Tu pasi ya kusafiria

0
17

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa kwa pasi za kusafiria za wataalamu wa kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini wanaojenga meli ya MV Hapa Kazi Tu jijini Mwanza hadi wakamilishe kazi yao.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo akizungumza na wananchi na viongozi wa mkoa huo mara baada ya kukagua ujenzi wa meli hiyo katika eneo la Mwanza South, wilaya ya Nyamagana.

“Nimemwagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa akamate pasi zao mara moja na ahakikishe hakuna mtu anatoka nje ya mkoa huu hadi hii kazi ikamilike. Nimeambiwa wako saba, lakini hapa wako watatu. Watafuteni hao wengine wako wapi,” ameagiza.

Wenye pasi hizo ni Meneja wa mradi, Dong Myung, na wasaidizi wake Kyungan Choi na Khuh Yun.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mwanza kwa ziara ya siku moja, amesema Serikali imeshalipa asilimia 80 ya gharama za ujenzi wa meli hiyo lakini kazi iliyofanyika kwa mujibu wa mkataba ni asilimia 65 tu. Amesema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa wafanyakazi walikuwa 118 lakini sasa wamebakia 22 tu.

“Nimeingia ndani kukagua kazi ya ujenzi lakini sijaridhika nayo. Katika maelezo yao nimebaini kuwa kampuni tuliyoingia nayo mkataba ya GAS Entec imeuza share zake bila Serikali kuarifiwa. Waliouziwa, walipokuja walishangaa kuona ujenzi wa meli kwa sababu suala la ujenzi liko nje ya mauziano yao.

“Hawa watu wasiondoke hadi kazi ikamilike na kama wataondoka basi  atakayewadhamini ni Balozi wao. Serikali tutaendelea kuwasiliana na Balozi wa Korea Kusini na tunaamini kazi hii itakamilika,” ameagiza Waziri Mkuu.

Send this to a friend