Mkuu wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Anna Gidarya amesema wazazi na walezi watakaobainika kushinda vilabuni na watoto wadogo na kuwanywesha pombe za kienyeji watachukuliwa hatua za kisheria.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo ambapo alisema kuna wimbi kubwa la wazazi hasa wanawake kwenda na watoto wadogo vilabuni kunywa pombe, na wakati mwingine huwanywesha ili wasiwasumbue wakati wakiendelea kunywa.
Aidha, Gidarya amewaagiza watendaji wote wa wilaya hiyo kufanya msako kwenye vilabu vyote vya pombe za kienyeji ili kuwakamata wanawake wote wanaofanya vitendo hivyo.
“Msako wa kuwakamata wanawake wote wanaokwenda na watoto vilabu vya pombe uanze mara moja, haiwezekani tuone watoto wetu wasio na hatia wanapata madhara ya kiafya kwa sababu ya ujinga wa wazazi wao, mnapenda kuona afya za watoto zinadhoofu na kupata udumavu sio?” alisema Gidarya.
Hata hivyo amewataka watendaji wa kata kufanya vikao vya mara kwa mara kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu athari za matumizi ya pombe kwa watoto wadogo utakaowasababishia udumavu, na kusisitiza elimu hiyo iwe endelevu.