Familia ya mfanyabiashara wa madini aliyeuawa yamtupia lawama Waziri Mkuu

0
24

Baada ya tukio la kuuawa kwa mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi Madola aliyedaiwa kuuawa na Polisi Mtwara Januari 5 mwaka huu na Serikali kuunda kamati maalumu ya uchunguzi, familia ya marehemu imemtupia lawama Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakidai kutoweka hadharani matokeo ya uchunguzi huo.

Familia hiyo imedai wamekuwa wakilala matanga kwa siku zaidi ya 126 na hawafahamu mwili wa mpendwa wao mahali ulipo na upo katika hali gani huku wakiiomba Serikali iwakabidhi mabaki ya mpendwa wao kwa ajili ya mazishi na kuhitimisha msiba.

Pia, wameliomba Jeshi la Polisi Mtwara kurejesha shilingi milioni 70 zilizochukuliwa kutoka kwa kijana wao, ambazo zinadaiwa kuwa chanzo kikubwa cha kuuawa kwake.

Aidha, mama mzazi wa marehemu, Hawa Ally amemuomba Waziri Mkuu Majaliwa ambaye aliunda kamati ya uchunguzi kuweka wazi ripoti hiyo hadharani ili ukweli ubainike.

“Kitendo cha tume ya Majaliwa kutotoa ripoti ya mauaji ya mwanangu, kinaibua maswali, naiomba Serikali itufahamishe kujua namna mambo yalivyokuwa tangu mwanangu alivyokamatwa na kilichosababisha kuuawa na kutupwa vichakani ili nyoyo zetu ziwe huru kuliko sasa,” amesema.

Hapo awali Polisi ilisema haiwezi kuukabidhi mwili kwa familia hadi ipokee ripoti kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, mbali na ripoti hiyo ilisema pia inasubiri maelekezo ya kamati mpya iliyoundwa na Waziri Mkuu.

Send this to a friend