Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda amefika katika Shule ya Msingi Mkonoo na kuzungumza na walimu pamoja na wazazi baada ya tuhuma ya wanafunzi 22 kudaiwa kulawitiwa na mmiliki wa madrasa.
Watoto hao wamedaiwa kulawitiwa na mmiliki huyo aliyejulikana kwa jina la Mzee Jumanne aliye jirani na shule hiyo huku mmoja akikutwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wengine tisa wakibainika kulawitiwa baada ya kufanyiwa uchunguzi hospitalini.
“Niliweka utaratibu wangu wa mtego wa kumkamata yule mtu anaye walawiti watoto wa shule ya msingi Mkonoo, lakini nilipoona mtego huu unachelewa nikaona ili tendo hili lisiendelee niliagiza watoto wale ambao wameshukiwa kulawitiwa wapelekwe hospitali, uchunguzi ufanyike halafu tupate ripoti, je matukio ya namna hii yanafanyika au hayafanyiki,” amesema.
Aidha, Mtanda amelaaani vitendo hivyo na kuagiza kusimamisha shughuli zote za shule kutokana na tuhuma na uchunguzi unaoendelea.
Pia, Mkuu wa Wilaya ameagiza kufungwa kwa madrasa hiyo huku mtuhumiwa akishikiliwa na polisi kwa mahijiano zaidi.